Jumamosi, 10 Novemba 2012

Kutokuwa Wabunifu ni Madhara ya Kufikiria Kijamaa?



Kumekuwa na mijadala mingi sana kuhusu watanzania wengi kutokuwa wabunifu ukulinganisha na nchi zingine majirani. Ukichukulia mfano wa Kenya, wakenya wamekuwa na biashara nyingi sana hapa kwetu ukilinganisha na zila za watanazania. Ukiangalia katika hali ya ubunifu na ujasiriamali kwa ujumla Kenya wanaonekana wako mbele sana ukilinganisha na sisi. Hata bidhaa zinazoingia Tanzania kutoka Kenya ni nyingi sana ukilinganisha na za watanzania zinazoenda Kenya.

Hivi ni kweli kuwa kutokuwa wabunifu kulisababishwa na fikira za kijamaa?
Kwa tafsiri rahisi ujamaa ni umilikaji wa njia za uchumi kwa pamoja. Wakati wa ujamaa mashirika yote ya umma yalimilikiwa na watanzania kwa pamoja. Mashirika kama RTC, UDA, NBC, NIC National Milling, n.k.yalimilikiwa na umma. Ilitegemewa mashirika haya yafanye biashara kisha yagawe gawio kwa serikali ili serikali nayo itoe huduma bure kwa wananchi. Hapa ndiyo dhana halisi ya ujamaa na umilikaji wa mitaji kwa pamoja ilipokuwa imejitika. Hivyo wananchi walitegemea serikali iwafanyie kazi katika mashirika yake na kuwapa mahitaji yao. Ndiyo maana kulikuwa na maduka ya kaya, mashamba ya pamoja ili uzalishaji uwe wa pamoja na kisha kugawana mazao. 

Bahati mbaya, kwa hapa kwetu dhana ya ujamaa haikuleta matunda yaliyotarajiwa. Mashirika yote yakafa baada ya watu wasiokuwa waaminifu kupewa kusimamia mashirika haya. Wakayafilisi yakaisha kabisa. Badala yake waliokuwa na dhamana ya kusimamia mashirika hayo wakajinufaisha na mashirika hayo mpaka yakashindwa kujiendesha. Itakumbukwa kuwa wakati wa awamu ya tatu utawala,  mashirika mengi yalikuwa yakitegemea ruzuku kutoka serikalini. Sasa badala ya mashirika haya kuilipa serikali gawio, serikali ikawa inayagharimia mashirika haya. Jambo hili halikuwa sawa ndiyo maana serikali ikayabinafsisha ili kuhamisha mizigo huo kwa sekta binafsi. 

Baada ya ubinafsishaji huu ambao ulisukumwa na dhana ya ubepari ulioingia Tanzania kimya kimya, wananchi hawakuambiwa kuwa umilikaji wa njia za uchumi kwa pamoja sasa basi hivyo watu waanze kukuza mitaji yao. Kuwa mitaji ile waliyoiweka katika mashirika ya umma kuanzia mwaka 1967 wakati serikali ilipowanyang'anya watu majumba na mali zingine ili zimilikiwe na serikali sasa imeisha. Kuwa kimya huku kumewafanya watanzania kuendelea kuelewa kuwa bado tuko kwenye ujamaa hivyo kutegemea serikali kufanya kila kitu. Kaulize vijana wale waliokaa vijiweni, stori ni serikali haijafanya hiki na kile. Serikali haitaweza kukufanyia chochote zaidi ya kuweka miundombinu na mazingira safi ya wewe kubuni na kuanzisha biashara yako. 

Katika kuwaelimisha watanzania kuanza kufikiria na kuwa wabunifu, serikali kwa nyakati tofauti ilitoa mbiu mbalimbali ili watu wazinduke. Kwa mfano kila kitu ni ruksa (Rais Mwinyi),  mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe (Rais Mkapa) na ile ya mabilioni ya JK( Rais Kikwete).  Hizi ni jitahada za serikali kusaidia watanzania kufuta kichwani mwao mawazo ya ujamaa na kuanza kukuza mitaji. Umiliki wa pamoja umeshaisha ndiyo maana hata shule hatuendi za aina moja, hospitali n.k. Hata hivyo juhudi hizi hazitoshi.  Urusi inatumia mabilioni ya dola kwa ajili ya kufuta fikira za kijamaa katika akili za warusi ili waweze kuanzisha na kukuza mitaji yao. Hapa kwetu mbiu tu hazitoshi, tufikirie kuwekeza katika kufuta fikira hizi zinazowafanya watanzania washindwe kuwa wabunifu na kuanzisha na kusimamia biashara zao. Lazima tuwekeze katika fikira sahihi kama tunataka watanzania watoke. 

Hali ya ujamaa imewapumbaza wengi  hata wasomi wetu hawawaelezi watanzania kilichotokea hapo katikati na kuanza kuwafundisha jinsi ya kubadili fikira na fahamu zao ili zijielekeze katika kuanzisha biashara na kuacha kuitegemea serikali kwa kila jambo. Hata nchi za wenzetu ambazo ujamaa umeshindwa wanatumia fedha nyingi sana kuwaelimisha wananchi wao kufuta mawazo ya kutegemea serikali na kuanza kukuza mitaji binafisi.

Sisi Elizabethrose Memorial Institute  tumeona kuwa watu kuendelea kutegemea serikali na kushindwa kubuni na kuanzisha biashara zao ni tatizo linalohitaji juhudi nyingi katika kulitatua. Hatuwezi kuiachia serikali ianze kuendesha mafunzo ya kufuta yale tuliyowaaminisha watanzania, na kuwaelimisha nguvu ya ujasiriamali na kufungua ufahamu wao.  Hatuhitaji kuingia katika mtego ule wa kuiachia serikali kila kiti isipokuwa tumeanzisha madarasa ya mafunzo ya ubunifu wa biashara, kusimamia na kuendeleza biashara. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni