Alhamisi, 8 Desemba 2011

MIAKA 50 YA UHURU NA MJASIRIAMALI


Tumedhubutu Tumeweza na Tunasonga mbele " ni kaulimbiu ya kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika.  Bado tuna safari ndefu ya kuwawezesha watanzania waliowengi kuweza kujiajiri na kuondoa utegemezi katika kusubiri kuajiriwa. Leo hata wale waliopata fursa ya kwenda shule hata kufikia elimu ya juu wanazunguka na vyeti vyao kutafuta ajira. Wasomi ni wengi ajira chache, wale wasopata bahati ya kwenda shule hata kufikia elimu ya juu ambao  ndio watanzania waliowengi wako kwenye hali mbaya zaidi ya kuweza kuajiriwa au kujiajiri. Katika msimu huu wa soko huria ufahamu na ubunifu wa hali ya juu unahitajika ili watanzania waliowengi waweze kujiajiri na kuwa wajasiriamali wenye mafanikio.

Tangu uhuru wa Tanganyika mfumo wa ujamaa  na kujitegemea ambao kimsingi ulikuwa na malengo mazuri, mitaji ilimilikiwa kwa pamoja, kulikuwa na maduka ya ushirika, vyama vya ushirika, shule za aina moja ili kuweka usawa kwa wote. Kwa upande mwingine mfumo huu ulidumaza fikra za watanzania walio wengi kujijengea utamaduni wa kuweza kumiliki mitaji yao binafsi  ili kuweza kujiajiri na sio kusubiri kuajiriwa.

Leo tunashaherekea miaka 50 ya uhuru  wa Tanganyika, kwa kiasi kidogo “Tumedhubutu Tumeweza na Tunasonga mbele " kumwezesha mtanzania kumiliki mtaji kwani watanzania walio wengi wameweza kuanzisha na kusimamia biashara zao, walio wachache wamekuwa wajasiriamali wakubwa wenye mafanikio hata kuweza kutoa ajira kwa wengine.

Serikali imejitahidi kuhamasisha wanachi kutotegemea zaidi kuajiriwa na badala yake wajiajiri ili kuweza kukabiliana na soko huria. Serikali pia, imetoa fursa mbalimbali ikiwemo kusaidia kifedha, Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa mstari wa mbele kwa kutoa ‘mabilioni ya JK’  na taasisi mbalimbali  za fedha wamejitahidi kuwawezesha wajasiriamali kwa kuwapa mikopo ili waweze kuendeleza biashara zao. Kutokana na utafiti wetu tuliofanya, bado masharti ya mikopo yameonekana kuwa ni magumu kwa wajasiriamali. Elimu ya ujasiriamali imekuwa inatolewa kwa kiasi kidogo sana.

Kutokana na utafiti tulioufanya katika taasisi yetu ya Elizabethrose Memorial Institute (EMI) kwa  mwaka huu kwa wajasiriamali na watanzania zaidi ya 100, tumegundua kuwa:
·         Mtazamo na ufahamu wa watanzania(mindset) ndio kiini cha watanzania waliowengi kushindwa kujiajiri, hata walioanza biashara(wajasiriamali) wamekwama, wanashindwa kuendeleza biashara zao, wamekata tamaa. Bado tuna kazi kubwa ya kuwawezesha watanzania kwanza kwa kukomboa fikra zao ili kubadili mtazamo(mindset yao) kujua kwamba wanaweza, wajiamini kwakuwa kila kitu kinaanza kama wazo. Tukiweza kuukomboa ufahamu wa mtanzania tutapiga hatua kubwa sana.

·         Nitaanzaje biashara bila mtaji? Nitapata wapi mtaji wakati masharti ya kupata mkopo ni magumu? Nitafanya biashara gani itakayokuwa endelevu? Haya ndio maswali ambayo watanzania wanajiuliza leo ambayo ndiyo yanawafanya washindwe kujiajiri au kuendeleza biashara zao. Ukweli ni kwamba yote yanawezekana wanahitaji kuelekezwa.

·         Wanashindwa kutumia fursa ya mikopo kwa hofu ya kushindwa kulipa riba au marejesho.

·         Wanafanya biashara kwa kuiga na sio kutokana na vipaji vyao hivyo kushindwa kuwa na biashara endelevu

·         Wanatumia vibaya mikopo wanayopewa hivyo kuishia kufilisiwa. Wanachanganya mtaji na matumizi binafsi.

Kutokana na utafiti huu, Serikali  inashauriwa iziwezeshe taasisi zinazotoa mafunzo ya ujasiriamali kwanza kubadilisha mtazamo(mindset) za watanzania waliowengi,  kuwapa elimu na mbinu mbalimbali za kuwa wajasiriamali wenye mafanikio. Ihamasishe masharti nafuu ya mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati.