Shauku ni kiu au hamu ya kutaka kukijua au kukipata kitu Fulani. Shauku inaweza ikaleta manufaa ikitumiwa vizuri. Leo ninapenda kuongelea shauku ambayo watu wengi wanayo ila mimi ninajikita zaidi katika ile shauku iliyojengwa katika misingi chanya zaidi kwa mfano, shauku ya kutaka kujua wewe ni nani na kusudi lako hapa duniani ni lipi?
Kila mwanadamu aliyeko chini ya jua analo kusudi lake aliloitiwa kulifanya hapa duniani, hili ni jambo la kulichunguza kwa umakini na kulipatia ufumbuzi, ninasema ufumbuzi kwa sababu kitendo cha wewe kutojifahamu au kutolitambua kusudi lako hapa duniani ni tatizo kubwa sana. Ukweli ni kwamba kila mtu analo eneo lake analotosheleza vizuri yaani analoweza kulifanyia kazi vizuri zaidi katika Nyanja mbalimbali.
Kabla ya kulijua eneo unalotosheleza ni vizuri uwe umepitia au umejiruhusu kuwepo katika mazingira yafananayo na eneo hilo kwa mfano, ili kujua kama wewe ni mzuri katika mambo ya saluni ni vizuri uwe umekaa maeneo ambayo shughuli zinazofanyika saluni huwa zinafanyika na hapo hata kama zinafanywa katika mazingira yasiyo rasmi. Ni vigumu kumkuta mtu aliyekulia katika jamii ambayo wanawake na wanaume wananyoa vipara vya wembe kila wakati na hawaamini katika kusuka au kutengeneza nywele kwa mtindo wowote ule akawa mtaalamu katika mambo ya urembo wa nywele, kama kuna watu kama hao, basi ni wachache sana.
Uzoefu unaonyesha kuwa watu waliozaliwa au kukulia maeneo yanayozungukwa au karibiana na vitu kama bahari, mito na maziwa ni wazuri sana katika kuogelea au shughuli zinazohusiana na uvuvi kuliko wale waliozaliwa sehemu kame.
Eneo unalotesheleza litaeleweka vizuri nikiliita “kipaji”. Kipaji chako ndio maisha yako, mtaji wako na ndio eneo lako litakalokutoa kimaisha, nikisema litakalo “kutoa” namaanisha litakalokusababishia upande au ufanye vizuri kimaisha. Kipaji chako kitakuwa na nguvu zaidi kikigunduliwa na wewe mwenyewe, na ili ukijue ni lazima uwe na “shauku” ya kukigundua hasa kwa kuanza kujichunguza ni kusudi gani unahisi unalo hapa duniani. Shauku yako ikiwa kubwa ndipo uwezekano wa wewe kugundua kipaji zaidi ya kimoja ndani yako unapotokea. Ni kitu gani hasa unapendelea kukifanya na unaweza kukifanya na unasikia amani na furaha kukifanya? Huenda hicho ndicho kipaji chako na kinahitaji kukuzwa. Kipaji ni zawadi aliyopewa mtu tangu kuumbwa kwake, sio kitu cha kuiga kutoka kwa mtu mwingine. Kipaji pia sio lazima kitokane na mazingira aliyokulia mtu kwani vitu vingine vinavyoitwa vipaji sio vipaji, ni ujuzi tu mtu aliojifunza au anaouiga na hii huwa haileti matokeo mazuri. Nahitimisha kwa kusema “kuwa na shauku ya kukijua kipaji chako”.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni