Jumanne, 13 Septemba 2011

VYOTE VILIANZA KAMA WAZO.

Je, umewahi kujiuliza ni kwa jinsi gani vitu vyote humu ulimwenguni viliumbwa? Je, wanadamu waliumbwa kutokea nini au wapi? Haya ni maswali ya muhimu ambayo wewe kama mwanadamu unapaswa kujiuliza na mwisho wa siku kupata majibu sahihi. Lengo langu hapa sio kujadiliana na wewe kuhusu vitu vilivyotumika kuutengeneza ulimwengu au kuwaumba wanadamu, la hasha, kwani kwa kufanya hivyo hatutaweza kuumaliza mjadala huo sababu nitakuuliza ni wapi hivyo vitu vilivyotumika kutengenezea (yaani malighafi) vilipotokea. Nia yangu ni kutaka kukushirikisha juu ya nilichogundua kuhusiana na ukweli huu kuwa “kila kitu kilianza kama wazo”.

Tukiuangalia uumbaji kutoka katika mitazamo ya baadhi ya dini zetu tunagundua kuwa wote na vyote ulimwenguni humu viliumbwa na Mungu. Bila shaka utakubaliana na mimi kuwa kabla Mungu hajaamua kuiumba dunia na wanadamu aliwaza kwanza. Aliuwaza uwepo wa nchi kavu ndipo akaziumba, aliuwaza uwepo wa makusanyiko yote ya maji yaani bahari, maziwa, mito na yote yafananayo na hayo ndipo alipoviumba. Hata wanyama na wanadamu vivyo hivyo, bila kusahau vitu vyote ambavyo wewe unaviita ni vya asili vilitokana na mawazo kwanza kabla ya kuumbwa kwake.

Tukiachana na uumbaji wa Mungu, hebu na tuuangalie uumbaji wa wanandamu. Vitu vyote visivyo vya asili vimetengenezwa na wanadamu wenyewe, kwa mfano nyumba kwa mitindo yake yote kuanzia maghorofa hadi zile za jadi. Magari, mavazi hata vyombo vya nyumbani ni baadhi tu ya vitu vilivyotengenezwa na wanandamu. Hebu ichunguze hiyo computer unayoitumia, hicho kiti ulichokikalia na hayo mavazi uliyoyavaa, umegundua nini? Hayo yote ni mawazo ya watu, kabla hawajavitengeneza  waliwaza kwanza. Kuwaza kitu ni kukiona hicho kitu kwa wakati ujao. Aliyegundua viatu alianza kuwaza  na ndipo aliwaona watu wamevaa viatu hata kabla viatu hivyo havijatengenezwa. Kila kitu unachokiona na kukitumia ni wazo la mtu, kilianza kama wazo, kikatendewa kazi ndipo kikadhihirika kuwa mali au bidhaa bora. Wazo lolote unalolipata litendee kazi pasipo kuyakaribisha mawazo hasi. Jaribu kuwaza hivi kama Mungu angewaza hasi kabla ya kutuumba, mimi na wewe tungeumbwa? Pamoja na ukweli kuwa mimi na wewe tunamkosea kila siku aliyetuumba, hiyo haijawa sababu ya yeye kujuta kutuumba na kuutowesha kabisa uumbaji wake badala yake wanadamu wazidi ongezeka. Je, kuna haja gani ya mimi na wewe kuyatowesha mawazo mazuri ya maendeleo eti kisa tu tunayaruhusu mawazo hasi akilini mwetu?

Ninahitimisha  kwa kusema kuwa kila mtu anaweza na anayo haki ya kuyafurahia matunda yatokanayo na mawazo na mitazamo yake. Hili litawezekana tu iwapo tutawaza kwa usahihi na kwa mitazamo chanya ya kijasiriamali daima.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni